Jeremiah 6

Yerusalemu Imezingirwa Na Jeshi


1 a“Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini!
Kimbieni kutoka Yerusalemu!
Pigeni tarumbeta katika Tekoa!
Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu!
Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini,
na uharibifu wa kutisha.

2 bNitamwangamiza Binti Sayuni,
aliye mzuri sana na mwororo.

3 cWachungaji pamoja na makundi yao
watakuja dhidi yake;
watapiga mahema yao kumzunguka,
kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.”


4 d“Jiandaeni kwa vita dhidi yake!
Inukeni tumshambulie mchana!
Lakini, ole wetu, mchana unaisha,
na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.

5 Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku,
na kuharibu ngome zake!”

6 eHivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Kateni miti mjenge boma
kuzunguka Yerusalemu.
Mji huu ni lazima uadhibiwe,
umejazwa na uonevu.

7 fKama vile kisima kinavyomwaga maji yake,
ndivyo anavyomwaga uovu wake.
Ukatili na maangamizi yasikika ndani yake,
ugonjwa wake na majeraha yake viko mbele yangu daima.

8 gPokea onyo, ee Yerusalemu,
la sivyo nitageukia mbali nawe
na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa,
asiweze mtu kuishi ndani yake.”

9Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli
kwa uangalifu kama kwenye mzabibu;
pitisha mkono wako kwenye matawi tena,
kama yeye avunaye zabibu.”


10 hNiseme na nani na kumpa onyo?
Ni nani atakayenisikiliza mimi?
Masikio yao yameziba,
Masikio yameziba kwa Kiebrania ina maana kwamba masikio yao hayajatahiriwa.

kwa hiyo hawawezi kusikia.
Neno la Bwana ni chukizo kwao,
hawalifurahii.

11 jLakini nimejaa ghadhabu ya Bwana,
nami siwezi kuizuia.

“Wamwagie watoto walioko barabarani,
na juu ya vijana waume waliokusanyika;
mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake,
hata nao wazee waliolemewa na miaka.

12 kNyumba zao zitapewa watu wengine,
pamoja na mashamba yao na wake zao,
nitakapounyoosha mkono wangu
dhidi ya wale waishio katika nchi,”
asema Bwana.

13 l“Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,
wote wana tamaa ya kupata faida zaidi;
manabii na makuhani wanafanana,
wote wanafanya udanganyifu.

14 mWanafunga majeraha ya watu wangu
bila uangalifu.
Wanasema, ‘Amani, amani,’
wakati hakuna amani.

15 nJe, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao
inayochukiza mno?
Hapana, hawana aibu hata kidogo;
hawajui hata kuona haya.
Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,
watashushwa chini nitakapowaadhibu,”
asema Bwana.

16 oHivi ndivyo asemavyo Bwana: “Simama kwenye njia panda utazame,
ulizia mapito ya zamani,
ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo,
nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita hiyo.’

17 pNiliweka walinzi juu yenu na kusema,
‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’
Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’

18 qKwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa,
angalieni, enyi mashahidi,
lile litakalowatokea.

19 Sikia, ee nchi:
Ninaleta maafa juu ya watu hawa,
matunda ya mipango yao,
kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu
na wameikataa sheria yangu.

20 rUnanifaa nini uvumba kutoka Sheba,
au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali?
Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki,
dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”

21 sKwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Bwana: “Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa.
Baba na wana wao watajikwaa juu yake,
majirani na marafiki wataangamia.”

22 tHivi ndivyo asemavyo Bwana: “Tazama, jeshi linakuja
kutoka nchi ya kaskazini,
taifa kubwa linaamshwa
kutoka miisho ya dunia.

23 uWamejifunga pinde na mkuki,
ni wakatili na hawana huruma.
Wanatoa sauti kama bahari inayonguruma
wanapoendesha farasi zao.
Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita
ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.”


24 vTumesikia taarifa zao,
nayo mikono yetu imelegea.
Uchungu umetushika,
maumivu kama ya mwanamke katika utungu wa kuzaa.

25 wUsitoke kwenda mashambani
au kutembea barabarani,
kwa kuwa adui ana upanga,
na kuna vitisho kila upande.

26 xEnyi watu wangu, vaeni magunia
mjivingirishe kwenye majivu,
ombolezeni kwa kilio cha uchungu
kama amliliaye mwana pekee,
kwa maana ghafula
mharabu atatujia.


27 y“Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma,
nao watu wangu kama mawe yenye madini,
ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.

28 zWote ni waasi sugu,
wakienda huku na huko kusengenya.
Wao ni shaba na chuma,
wote wanatenda upotovu.

29 Mivuo inavuma kwa nguvu,
kinachoungua kwa huo moto ni risasi,
lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure;
waovu hawaondolewi.

30 aaWanaitwa fedha iliyokataliwa,
kwa sababu Bwana amewakataa.”
Copyright information for SwhKC